ROZARI TAKATIFU NA ROZARI HAI



ROZARI HAI
(a)Historia
Karne ya 18 LionsUfaransa.
Paulina alitekwa na wazo namna ya kuwashawishi watu kupenda kusali Rozari ambayo imekuwa ikisaliwa na wazee na wacha Mungu wachache.  Ibada ya Rozari ilielekea kuwa  imepitwa na wakati  katika maisha ya wengi. Kulikuwa na watu wachache waliokuwa wakijitahidi katika ibada hii lakini mshikamano wao haukuwa wa uhakika kutokana na wimbi la wakati huo kuwa starehe iliwekwa mbele. Paulina alielewa ibada binafsi za watu hao wa pekee ni kama “cheche bila kuhusisha wengi katikati ya giza nene.”
Kinachohitajika katika giza nene siyo cheche bali mwanga; Mwanga unaoishi au Mwanga wa kudumu”
LINAFANYIKAJE HILO?
Tunakusanya cheche mpaka kuzifanya mwanga unaoishi.
(ROZARI HAI )-Mwanga uliounganika unaoishi na kuwaka katika upendo  na kwa upendo.
Kupitia sala zake Paulina  - Mungu alimwonyesha  Paulina njia-RAHISI SANA
KUGAWA ROZARI KATIKA VIPANDE 15  kwa sasa  20 SAWA NA MAFUMBO 15 kwa sasa  20 YA ROZARI TAKATIFU.
Kwa jinsi kwamba kila mtu  atasali kumi moja tu na kutafakari fumbo husika la kumi hiloROZARI HAI- Hii siyo  ibada ya mtu binafsi ni sala ya familia, familia inayoasali kila siku. Mt 18:19 -20 mdo 1:14
Mwenye heri Paulina alianzisha Rozari Hai 1826  Ilitambuliwa  rasmi na kujazwa Rehema nyingi  na  Papa Gregory 16 na kuwekwa katika kitabu cha sheria za kanisa tarehe 27/1/1832
Rejea- “Faraja  ya uponyaji wa Moyo wa Maria uk 3 sura ya 3, ya 4 na ya 5.

(b)Rozari Takatifu na Rozari Hai.
Wazo la kupata ufafanuzi kuhusu tofauti kati ya Rozari Takatifu na Rozari Hai ni zuri na la msingi. Kimsingi hakuna tofauti  kati ya Rozari na Rozari Hai.Ni Rozari ile ile ya Mama yetu, ambayo imezoeleka katika Kanisa Katoliki, ikisaliwa na mtu binafsi au jumuiya.

Sasa katika Rozari Hai, ni Rozari ile ile inayosaliwa lakini sasa kama chama cha kitume  kijulikanacho kama ROZARI HAI.

Kama chama cha kitume, Rozari Hai inalenga kimsingi kusali Rozari kama FAMILIA YA KIROHO. Kwa mantiki kwamba, ingawa wana Rozari Hai, kimwili wametawanyika katika sehemu mbalimbali ulimwenguni, kwa majitoleo yao binafsi katika sala wanakuwa pamoja kama familia ya kiroho.

Kwa majitoleo binafsi katika kusali Rozari muhusika anaweza kusali kwa nia yake maalum lakini katika Rozari Hai, tunasali kwa nia kuu mbili:

1.   Ushindi wa Moyo Imakulata wa Maria.
2.   Kwa heshima ya Mt. Filomena.

Hivyo hizi nia za msingi pamoja na upendo wetu katika kuwajali wengine katika shida zao, tunaunganika pamoja kama familia moja inayomwelekea Mama Maria, chini ya usimamizi wa Mt. Filomena.

Wanachama wa Rozari Hai, wana wajibu wa kusali kwa tafakari fungu moja tu la Rozari kila siku. Kwa kuwa ni jumuiya au familia iliyounganika katika nia na matendo ya huruma, sala ya kila mmoja inakuwa sala ya wote. Hii ina maana kwamba kila mwanachama, kiroho anasali mamilioni au mabilioni ya mafungu kila siku na kushiriki kikamilifu zawadi zote za kiroho zitokanazo na sala hizo.

NAMNA YA KUSALI:
1.    Kila Mwanachama atapewa fungu moja la Rozari la kusali kila siku
2.    Kila Mwanachama atapewa fumbo la kutafakari kila asalipo Rozari (fungu lake).
3.    Akumbuke kutolea nia za msingi zilizotajwa hapo juu.

                MFANO: Mimi binafsi naweza kupiga magoti chumbani mwangu nikasali mafungu yote ishirini ya Rozari. Ni mimi peke yangu nasali yale mafungu ishirini, kwa nia zangu binafsi na hatimaye nitapata mastahili ya mafungu ishirini tu. Sasa, katika Rozari hai, kila mwanachama anayesali fungu moja ni kama anasali mamilioni ya mafungu kwa sababu wanachama wote wameunganika kuwa kitu kimoja (mmoja) kiroho, katika Moyo Imakulatawa Maria wakisali popote walipo kwa:

-      Sauti moja
-      Akili moja
-      Moyo mmoja
-      Nia moja
-      Kama familia moja

Kwa hiyo, mambo hayo makuu matano, ndiyo kwa kiasi Fulani yanatofautisha kati ya Rozari Hai na ile ya kawaida.

Hivyo, Rozari Hai ni namna ya kusali Rozari yenye nguvu sana na faida zaidi. Ndiyo maana Papa Gregori wa 16 na wengine waliofuatia baada yake hawakusita kuipitisha kwa ajili ya kanisa zima.
                
Ukweli ni kwamba majitoleo ya roho moja moja zilizotengana ni kama cheche ya moto katikati ya giza nene, ambayo huwaka bila kutoa ndimi za moto. Lakini kwa njia ya umoja wetu wa upendo katika kusali Rozari Hai,hizi cheche zinaunganika pamoja na kuwa moto uwakao daima bila kuzimika. Ndiyo maana tunaita Rozari Hai kwa sababu ni moto unaowaka ukitoa mwanga tofauti na cheche ya moto ya mtu mmoja mmoja: kwa Kiswahili tunasema UMOJA NI NGUVU. Na kwa kuwa wanachama wake wote wameunganika kwa ujumla katika hii Rozari Hai kokote walioko basi kwa ujumla tunaiita CHAMA CHA UTUME WA ROZARI HAI YA MT. FILOMENA MAHALI POTE.

Kila Mwanachama wa Rozari Hai ni Mmisionari, kwa kuwa anasali kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Hii ndiyo maana ya USHINDI WA MOYO IMAKULATA WA MARIA. Na ndiyo hasa Yesu alimaanisha katika sala yetu ya Baba yetu: UFALME WAKO UFIKE, UTAKALO LIFANYIKE DUNIANI KAMA MBINGUNI. Kila Mkristu Mkatoliki anayehusudu wokovu wa Dunia, anayelipenda kanisa, Mama yetu Bikira Maria, na anayeamini nguvu ya Rozari, si rahisi kukataa kujiunga na Rozari Hai. Hivyo basi uanachama uko wazi kwa wote bila kujali umri: Hakuna mipaka katika idadi, kwani hadi sasa idadi inafikia zaidi ya wanachama milioni kumi na sita ulimwenguni. Kati yao wakiwemo maelfu ya Mapadre, Masista na idadi nzuri ya Maaskofu. Askofu Telesphore Mkude ni Askofu wa kwanza Tanzania kuwa Mwanachama wa Rozari Hai.

Wanachama wote wanaandikishwa rasmi na kupewa kadi ya fungu la kusali. Ni matarajio yetu kwamba maelezo haya yatawatia moyo kuitangaza Rozari Hai kama habari njema katika sehemu zenu.

 Wanachama wa Rozari Hai hawahitaji kukusanyika ili kusali mafungu yao. Mtu anaweza kusali wakati wowote mahali popote, usiku au mchana – ili mradi asali fungu lake kadri atakavyoona inafaa.

Hata hivyo, kama chama cha Rozari na mfano wa familia, wanachama katika kila Parokia au Kigango wanapaswa kukutana walau mara moja kwa mwezi Kanisani  ili kutiana nguvu na moyo wa kusali mafungu yao, na pia kutumia muda huo kutia uhai katika utume mbalimbali walionao. Na hapa inapendekezwa wakutane Jumapili ya tatu ya kila mwezi.

Utume mbalimbali tulionao katika Rozari Hai ni:
Wanachama kusali  kila siku fungu la Rozari walilopewa, wakitafakari juu ya fumbo husika walilopewa kila mmoja.(Hili ni la msingi)

Halafu kuna;
1.    Kutembelea wagonjwa nyumbani na hospitalini.
2.    Kuwasaidia wale wanaohitaji msaada wa kiutu.
3.    Kuhimiza majitoleo kwa Mama yetu kwa kufanya semina na mikutano.

Kwa hiyo kuna utaratibu kwamba katika kila sehemu ambako tuna wanachama, kunapaswa kuwa na watu kati ya watano (5) na saba (7) kama viongozi, wakishirikiana na wanachama. Ambao ni; Mwenyekiti, Makamo Mwenyekiti, Katibu, Makamo katibu, Mhazini, Mkutubi na Mratibu.

Hapa chini ni utaratibu wa sala wa kila mwezi wa kusali katika kusanyiko la wana Rozari Hai:
1.    Kwa jina la Baba ………………………………
2.    Uje Roho Mtakatifu (au wimbo wa Roho Mtakatifu)
3.    Rozari ya makumi matano
4.    Litania ya Bikira Maria
5.    Wimbo wa Bikira Maria
6.    Tasbihi / Taji dogo la Mt. Filomena
7.    Litania ya Mt. Filomena
8.    Wimbo wa Mt. Filomena
9.    Sala za Mt. Filomena
10.  Mazungumzo ya kiroho (dakika 5 – 10)
11.  Sala za kukua kwa Rozari Hai katika Parokia, Jimbo na Taifa.
-              Baba yetu x 1
-              Salaam Maria x 3
-              Atukuzwe Baba x 1
12. Sadaka
13. Mazungumzo, taarifa, kugawa wajibu mpya, nk.
14.  Matangazo
15.  Sala za kufunga
·               Kuwaombea wagonjwa na wenye shida mbalimbali
-        Baba yetu x 1
-        Salaam Maria x 1
-        Atukuzwe Baba x 1
-        Salaam Malkia

Licha ya mikutano ya sala, huwa tunafanya NOVENA kabla ya sikukuu au sherehe za Bikira Maria kama: Jan. 10, Machi 25, Mei 13, Julai 16, Agosti 11 na 15, Oktoba  7  na Disemba 8.

(c)Namna ya kusali kumi lako.
Sala
Tuungane na wanachama wa Jumuiya ya  Rozari Hai Duniani kote na kutolea fungu hili la Rozari Takatifu kwa;  Ushindi wa Moyo Imakulata wa Maria, kwa heshima ya Mt. Filomena,  Paulina Jaricot,na   Mt.Theresia ;   Kwa ajili ya Maaskofu  wote,  Mapadre na  Watawa,  wanachama, wagonjwa  na wanaoteseka;  watakaokufa leo ili wapewe neema ya uvumilivu na hatimaye kifo chema , pia kwa ajili ya amani katika familia zetu.

………………KUMI LANGU…………………….…                                                                  (hapa Sali kumi lako)
Kumi linajumuisha; Fumbo husika,  Baba yetu  x 1,   Salamu Maria  x 10  -zikiambatana na tafakari ya fumbo husika,   Atukuzwe Baba  x 1  na  Ee Yesu mwema…….   .
                          …………………………………………………………………….
                                                   (Kisha endelea na sala hii )

Ee Maria uliyeumbwa pasipo dhambi ya asili, tunaomba kwako upendo mkamilifu kwa Yesu Kristu !
Ee Roho Mtakatifu nakutolea  Moyo wa Kiekaristi wa Yesu, Damu yake Takatifu;  Moyo Imakulata  wa Maria wenye uchungu, mpole, mnyenyekevu na mtii, kulipia makosa yangu yote na madharau yangu. Najitolea kabisa  kwako. Naweka matumaini  yangu yote kwako.  Amina.
Tafakari ----Rejea kijitabu “FARAJA YA UPONYAJI WA MOYO WA MARIA  Uk.8
(a) Rehema kwa wanachama wa Rozari Hai.
                                   
Kwa kusali Rozari hai tunaweza kujipatia rehema nyingi sana, ambazo tunaweza kuzitolea kwa ajili ya roho  za Toharani.  Nazo ni kama zifuatazo.
1.      Rehema kamili siku ya kupokelewa katika ushirikawa Rozari hai.

2.      Rehema kamili kila jumapili ya tatu ya kila mwezi na pia siku za sikukuu ya Yesu na Bikira Maria.

3.      Rehema kamili siku za sikukuu zifuatazo:  Epifania, Ekaristi, Utatu Mtakatifu, Watakatifu Petri na Paulo na sikukuu ya Bikira Maria wa mlima Karmeli.

4.      Rehema  kamili saa ya kufa.

5.      Rehema zote zilizotolewa kwa wenye kusali Rozari nzima (Tasbihi nne).

6.      Rehema nyingine nyingi sana, ambavyo ni vigumu kuziorodhesha hapa zote.

-Rejea kijitabu-“ Faraja ya Uponyaji wa Moyo wa Maria” Uk6 sura ya 8

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

ROZARI TAKATIFU

MATOKEO YA FATIMA