ROZARI TAKATIFU



                                                          Historia
Rozari ni taji la Mawaridi.Ni neno la kilatini lenye maana ya Bustani ya maua ya waridi.
Rozari inahusishwa na Zaburi 150 ambazo Wayahudi walizitumia kama sala hekaluni.
Karne ya 12 walizuka wazushi wapinga dini, walioitwa Waalbigensia. Hawa walienea Kusini ya Ufaransa na Kaskazini ya Italia.
Baba Mtakatifu wa wakati huo alimteua Padre Dominiki awahubirie.  Aliwahubiria kwa maarifa yake yote lakini walizidi kushupaa na kumdhihaki. Mt.Dominiki alipoona kuwa uzito mkubwa wa dhambi walizotenda watu unazorotesha kuwageuza Waalbigensia, alikwenda msitu wa Toulouse na kusali mfululizo kwa siku tatu usiku na mchana.  Akiwa msituni alijitesa vikali ili kuomba huruma ya Mwenyezi Mungu.
Alijitesa kiasi kwamba alijipiga mijeledi mwishowe alizirai kabisa. Mama yetu alimtokea akiwa na Malaika watatu na kumwambia: “Mpendwa Dominiki, je, unajua Utatu Mtakatifu unataka kutumia chombo gani kuurekebisha ulimwengu? ’’ Mt. Dominiki alijibu: “ Wewe unaelewa zaidi kuliko mimi maana wewe uko karibu zaidi na Mwanao Yesu Kristu na umekuwa nyenzo kuu ya wokovu wetu”. Bikira Maria alimjibu: “Nataka ujue kuwa katika vita kama hivi ukitaka kuvishinda, hubiri Rozari yangu; ukitaka kuishinda mioyo migumu na kuirejesha kwa Mungu, hubiri Rozari yangu.’’
Baada ya Dominiki kuihubiri Rozari na kusali Rozari, wazushi zaidi ya laki moja waliongoka.(Rejea: Siri ya Rozari,  uk.24-26)
Toka hapo sala ya Rozari ilipata kuenea upesi sana popote Duniani, na waumini kuisali sala hiyo kwa bidii na juhudi kubwa sana.
                                                                                   
Sala ya Rozari Takatifu inahitaji unyenyekevu mkubwa. Katika kusali Rozari unarudiarudia mambo unayoyajua na kuyafahamu. Wenye majivuno wanaidharau, lakini wanaompenda Bikira Maria na Mungu wanaithamini sana. “Ni nani kama Mungu wetu aliyekaa juu na anawaangalia walio chini, mbinguni na duniani?”(Zaburi 113;5-6)
 Sala ya Rozari ni mwigo wa wimbo wa Malaika wakuu wanaosimama mbele ya kiti cha enzi cha Mungu wakiimba kwa kupokezana: Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi, mbingu na nchi zimejaa utukufu wako. Siri hii ya kiti cha enzi cha Mungu imefunuliwa (Isaya 6:3). Vivyo hivyo wenye kusali sala ya Rozari Takatifu ya familia au ya jumuiya wanapokezana kumsifu Mama Bikira Maria. Je, si vema na sisi pia kumtukuza Mama wa Mungu vile kama hao Malaika wakuu? Ameshuhudia mwenyewe jinsi anavyoipenda sala hii alipomtokea Mtakatifu Bernadetta Soubiru huko Lourdes, Ufaransa ya Kusini tarehe 11/2/1858 mpaka 16/7/1858. Alikuwa ameshika Rozari mikononi mwake. Akasali pamoja na huyo binti mpendevu wake.
Alitabasamu wakati huyo binti alipomsalimia kwa ‘Salamu Maria’. Alimtukuza mwanaye hapo sala ya ‘Baba yetu’ iliposemwa; lakini alijiunga na Bernadeta kusali ‘Atukuzwe Baba’.
Nov. 1877, Papa Pius wa tisa alisema: “Nawahimiza msali sala ya Rozari Takatifu kwa sababu ni Mama wa Mungu mwenyewe aliyetufundisha jinsi ya kuisali”.
Mwenyeheri Alan anasema: “Sala ya Rozari Takatifu ni hazina kubwa ya Neema; na wakosefu wengi wamepata wokovu kwa njia yake. Ni njia ya ajabu madhubuti ya kubatili dhambi na kujipatia neema”.  Baba Mtakatifu Gregori wa XIV alisema: “Sala hii inaongeza fadhila za watu wema.”
Naye Baba Mtakatifu Leo wa XIII aliongeza:
Ni jambo la ajabu sana kwamba watakatifu wote walioishi baada ya sala hiyo kufundishwa na Mtakatifu Dominika; waliisali sala hiyo kwa uaminifu mkubwa, Nayo ikawajalia nguvu kubwa ya kujitakasa”.
 Mtakatifu Fransisko wa Sale na Mtakatifu Alfonsi wa Ligori waliweka nadhiri ya kusali sala ya Rozari Takatifu kila siku kwa ibada kubwa.
Baba Mtakatifu Pius wa V na Mtakatifu Karoli Boromeo ingawa walikuwa na shughuli na kazi nyingi kila siku, hawakuacha kuisali kila siku; isitoshe waliisali katika jumuia pamoja na wenzao.
Mtakatifu Karoli Boromeo, aliwataka na kuwalazimisha wanafunzi wa seminari kuisali sala ya Rozari Takatifu kila siku. Mwenyeheri Klementi Hofbaure aliisali kila siku na kila mara alipokuwa faraghani, haswa alipokuwa akipita katika mitaa ya mji wa Vienna aende kuwahudumia wagonjwa. Sala hiyo ilimpatia waongofu wengi. Alizoea kusema: “Kila mara niliposali sala ya Rozari Takatifu kuomba wokovu wa watu wenye dhambi, sala yangu ilisikilizwa”
Kuna watu waliita sala ya Rozari Takatifu kuwa ni “Kipimo cha hali ya Ukristu (“Thermometer of Christianity”) kwa kweli hawakukosea. Tazama! Pale iliposaliwa kwa ibada na uaminifu mkubwa, utaona matokeo na matunda mazuri ya maisha ya Kikristu. Imani inasitawi na kutawala. Pale inapodharauliwa, unaweza kubashiri uchakavu na kupooza kwa maisha ya Kikristu. Mazoea ya kusali sala ya Rozari ndiyo sababu pekee inayodumisha hazina ya imani kwa karne nyingi.
Nyakati za maafa makubwa, waumini, kwa kusali sala ya Rozari Takatifu, waliweza kupata misaada ya ajabu na wakati mwingine miujiza. Ushindi wa vita vya Lepanto, mwaka 1571, usingalipatikana kama watu wasingesali sala hiyo ya Rozari. Ushindi wa Belgrade, mwaka 1716, nao ulipatikana kwa kusali Rozari. Yasemekana vema kwamba, maadui walipigwa zaidi kwa punje au shanga za Rozari kuliko kwa risasi za maaskari. Baba Mtakatifu Gregori wa XIII alifahamu jinsi ushindi huo ulivyopatikana kwa njia ya kusali Rozari Takatifu. Akaamuru sikukuu ya Rozari Takatifu iadhimishwe tarehe 7 ya mwezi Oktoba.
Baba Mtakatifu Sixtus IV alisema “Sala ya Rozari iliuepusha ulimwengu na majanga makubwa yaliyokuwa yakiuogofya; ilituliza hasira ya Mungu.”
Baba Mtakatifu Gregori wa XIII naye alisema wakati Mtakatifu Dominiki alipotumia sala ya Rozari ilikomesha maovu ya nyakati hizo, na kwamba sala hiyo ina uwezo wa Kimungu.


Baba Mtakatifu Leo XIII, tarehe 1/9/1883, alitilia mkazo mkubwa uwezo na uhakika wa sala ya Rozari kutokana na kushinda maovu ya nyakati zake. Naye Baba Mtakatifu Pius wa IX alirudia kusema: “Wanangu nisaidieni kushinda maovu ya kanisa na ya jumuiya, si kwa upanga, bali kwa sala ya Rozari Takatifu.” Nguvu za sala hiyo zaweza kujulikana na tu kwa ibada kubwa. Hakuna sala nyingine yeyote inayoweza kumtuliza mtu katika majonzi na dhiki au inayoweza kuondoa mahangaiko na fadhaa kuliko sala ya Rozari Takatifu. Sala ya Rozari ambayo inaitwa “Injili ndogo” inampa mtu anayeisali vema na kwa juhudi kubwa amani inayoahidiwa katika Injili.
Baba Mtakatifu Leo wa XIII aliamuru kuutolea kwa miaka yote mwezi wa Oktoba uwe mwezi wa Rozari Takatifu. Naye Baba Mtakatifu Pius wa IX aliacha kama wosia wake kwa waumini wote: “Salini pamoja kila jioni katika familia zenu sala ya Rozari Takatifu: Sala hii ni nyepesi na nzuri, iliyo na wingi wa Rehema, ni   wosia wangu wa mwisho ninaowaachieni. Siku moja pia aliwaonyesha waumini Rozari yake akisema: “Hii ndiyo Hazina kubwa ya Vatica.”  Ingekuwa jambo la maana sana na la kufaa kama kila mmoja wetu angaliweza kuinua na kuonyesha Rozari yake akasema kwa makini na moyo wote: “Angalieni hazina yangu kubwa ya nyumba yangu.”   Naye baba Mtakatifu Yohani Paulo wa II, kwa kuona umuhimu wa Rozari Takatifu aliongeza mafumbo matano ya Mwanga.
Mama Bikira Maria amekuwa akitokea katika matukio mbalimbali duniani, lakini kubwa na yenye msisitizo ni yale matokeo ya Fatina 1917. Katika  Tokeo la sita na la mwisho kule Fatima, 13/10/1917  B. Maria alisema Watu waendelee kusali Rozari kila siku” ;  Hivyo sharti tusali Rozari.

(b) Muundo wa Rozari Takatifu.
       i.            Kanuni ya Imani“Nasadiki kwa Mungu…….
Rejea Siri ya Rozari  uk. 55-56  Biblia  heb 11:6

     ii.            Baba yetu“Sala ya Bwana”
Ni sala aliyofundisha Mungu.
Rejea Siri ya Rozari-  uk. 57-72
Rejea Biblia - Mt.6:9-13
  iii.            Salamu Maria“Maamkio ya Malaika
Rejea Siri ya Rozari  uk. 72-85
Biblia- Lk 1:28, Lk 1:42

  iv.            Atukuzwe Baba………
Kuutukuza Utatu Mtakatifu.

    v.            Ee Yesu Mwema……..
Sala aliyotoa B. Maria  Fatima 13/7/1917 kuomba kwa Yesu atuepushe na moto wa Jehanamu.

(a) Matendo ya Furaha.( J.tatu na J.mosi)
 1.Maria anapashwa habari na Malaika.  ( Lk.1:28)
2.Maria alipoenda kumtembelea Elizabeti.  ( Lk. 1:41-42 )
3.Yesu anazaliwa Betlehemu.     ( Lk.2:7 )
4.Yesu anatolewa hekaluni.        ( Lk. 2:22-23 )
 5.Maria anamkuta Yesu hekaluni.      ( Lk. 2:46 )

     (b) Matendo ya uchungu.(J.nne na Ijumaa )

1.Yesu anatoka jasho la damu.    ( Lk. 22:44-45 )

2Yesu anapigwa mijeledi.     ( Yn. 19:1 )

3.Yesu anavikwa taji la miiba kichwani.   ( Mt. 27:28-29 )

4.Yesu anachukua msalaba.        ( Yn. 19: 17 )

5.Yesu anakufa msalabani.      ( Lk. 23: 46 )

( c )Matendo ya utukufu.       ( J.tano na J.pili )                                                          
1.Yesu anafufuka.    ( Mk. 16: 6 )
      2.Yesu anapaa mbinguni.    ( Mdo. 1:9-11 )
      3.Roho Mt. anawashukia mitume.    ( Mdo 2:2- 4 )
      4.B.Maria anapalizwa mbinguni.      ( 1 The 4:14-17 )
      5.Maria anawekwa malkia mbinguni.    ( Ufu. 12:1 )

( d ) Matendo ya Mwanga. ( Alhamisi )
        1.Yesu anabatizwa mtoni Yordani.    ( Mt. 3:16-17 )
        2.Yesu anageuza maji kuwa divai huko Kana.   ( Yn. 2:3-5 )
        3.Yesu anatangaza ufalme wa Mungu.    ( Mk. 1:14-15 )
        4.Yesu anageuka sura.    ( Mt. 17: 1- 2 )
        5.Yesu anaweka Ekaristi Takatifu.    ( Lk.22; 19- 20 )

Kusali Rozari ni kutafakari Maisha,Mateso,  kifo na utukufu wa Mkombozi wetu  Yesu Kristu.
Yote haya yapo kwenye Biblia Takatifu.
Rozari siyo mkusanyiko wa Baba yetu na Salamu Maria nyingi ila ni muhtasari
Mtakatifu wa mafumbo ya maisha, mateso kifo na utukufu wa Yesu na Maria.
Msomi Kajetani anasema…… kuacha kusali sala ya Baba yetu na salamu Maria ni kudondoka katika chambo cha  ndoto za shetani.
Sala hizi ni kinga nguvu na usalama wa mioyo yetu.
B. Maria alimweleza Mt. Getruda   Hapajatokea binadamu yeyote aliyeweza kumtungia kitu chochote kilicho kizuri kama “Salamu Maria
“Hapatakuwepo na maamkia yoyote yenye thamani katika moyo wangu kama uzuri na heshima  iliyopo katika maneno hayo yaliyotoka kwa Mungu Baba.”
Rozari ina sehemu kuu mbili:-
(a) Tafakari

(b) Kusema kwa Sauti
Rejea –Siri ya Rozari uk.  22.
Rejea- Siri ya Rozari uk. 97

Comments

Popular posts from this blog

ROZARI TAKATIFU NA ROZARI HAI

MATOKEO YA FATIMA